News

Uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti Kuhusu Hali ya Upatikanaji wa Elimu Bora kwa Watoto Wanaoishi katika Makazi Duni na yasiyo rasmi Mijini.

Asasi ya Kiraia ya HakiElimu imezindua Ripoti ya Utafiti kuhusu hali ya upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wanaoishi katika Makazi duni na yasiyo rasmi, Mijini ambao unatarajia kusaidia kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto wanaoishi katika makazi duni nchini Tanzania.

Utafiti huo wa HakiElimu umefanywa kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Afrika ‘APHRC’, chenye makao yake makuu jijini Nairobi ambapo utafiti huo umefanyika mwaka 2022 katika mazingira duni ya mijini na umeifikia mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.

Akizungumza wakati akizindua ripoti hiyo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Mkurugenzi Uthibiti Ubora, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ndg. Ephraim Simbeye amesema mpango wa Maendeleo ya Sekta Elimu wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26 unagusia Elimu ya mjini.

“Mpango huu unatambua kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaohamia mijini kutoka vijijini hali ambayo imesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi mijini ukilinganisha na vijijini. Kutokana na hali hii, utafiti huu unatuimiza kuanza kuitumia dhana ya Elimu ya mjini katika mipango yetu”.

Ndugu Simbeye ametoa wito kwa HakiElimu na wadau wengine kuendelea kufanya tafiti na kuziwasilisha kwa umma kwani unatoa nafasi kwa wadau mbalimbali pamoja na Serikali kutumia matokeo yake katika kufanya maamuzi ambayo yanajengwa katika Ushahidi wa Kisayansi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt John Kalage amesema HakiElimu ilisukumwa kufanya utafiti huo kwa lengo la kupata hali halisi ya upatikanaji wa elimu katika maeneo ya mijini na kuikuza dhana ya elimu ya mjini “Urban Education” kama eneo la kitaaluma na utafiti.

“Mara zote inaelezwa kuwa shule za vijijini zina changamoto kubwa kuliko za mjini na haziwavutii walimu kutokana na usafiri mbaya na huduma duni za kijamii , Pia inaelezwa kuwa utendaji wa wanafunzi vijijini upo chini ukilinganisha na mijini. Hata hivyo, mtazamo huu si sahihi sana kwani shule za mijini pia zina wanafunzi wenye utendaji wa chini. Miji ina changamoto zake zinazofanana na za vijijini” alisema Dr. Kalage

Naye Mwakilishi wa Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Afrika ‘APHRC’ Ndugu Francis Kiroro ametaja sababu za uchaguzi wa maeneo yaliyofanyika utafiti huo “Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050, asilimia 55 ya watu Tanzania watakuwa mijini, huku Dar Es Salaam ikiongoza kwa ongezeko la watu mijini baraka Afrika, hivyo mipango madhubuti inahitajika”

Utafiti huu ulifanyika katika Jiji la Dodoma, kata ya Chang’ombe na Jiji la Dar-es-Salaam katika kata za Kipawa , kata ya Kiburugwa katika Manispaa ya Temeke na kata ya Hananasifu Manispaa ya Kinondoni, amedokeza Ndugu Francis Kiroro.

Uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa Elimu ya Uraia Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana Katika Mchakato wa Kidemokrasia

Utafiti uliofanywa na asasi ya kiraia ya HakiElimu umeonesha kuwa sehemu kubwa ya walimu ambao wanafundisha somo la uraia hawana maarifa stahiki yanayowawezesha kuwafundisha na kuwaaandaa vijana ngazi ya sekondari katika kuelewa maana ya siasa safi na umuhimu wa ushiriki wao katika mifumo ya kidemokrasia katika ngazi ya shule, familia na jamii. 

Hali hii ni kinyume na matarajio ya wanafunzi hawa ambao kwa upande utafiti huu umeonesha kuwa wanategemea shule kama njia kuu ya kujifunza na kujengewa uzoefu katika michakato ya kidemokrasia ukilinganisha na vyanzo vingine mfano radio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na kujisomea vitabuni. 

Utafiti huo pia umeonesha kuwa somo la uraia halichukuliwi kuwa ni la umuhimu na lazima shuleni kwa sababu Mwalimu yoyote anaweza kufundisha somo hili pasi kulisomea na pia limetengewa muda mchache wa kujifunza kama ilivyo kwa masomo ya hiyari ya muziki na dini.

The State of Violence against School Children in Mainland Tanzania Report Launching

Hali ya Ukatili dhidi ya Watoto wa Shule Tanzania Bara’, ambao  umefanyika mwaka 2019.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalage wakati wa uzinduzi  wa Utafiti  huo jijini Dar es salaam amesema dhumuni kuu la Utafiti huo lilikuwa ni kupata taarifa rasmi na kujifunza hali halisi kuhusu ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto shuleni, pamoja na kuelewa vyanzo vya ukatili huo na kuboresha ulinzi na usalama wa watoto walio shuleni Tanzania Bara.

Utafiti huo umefanyika kwenye Wilaya 32 za  Tanzania Bara na kuzifikia shule 128, na unaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu kwenye mazingira salama shuleni na nje ya shule, hususani Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Unyanyasaji wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) (2017/18 – 2021/22).

Matokeo ya utafiti yameonyesha uwepo mkubwa wa matukio ya unyanyasaji wa watoto katika mifumo tofauti. Na takribani asilimia 87.9 ya watoto wote walio sailiwa, wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili ( physical violence), hususani kupitia adhabu za viboko.

Pia Utafiti umeonyesha kuwa asilimia 17.0 ya watoto walio shule za umma na asilimia 14.3 walio shule binafsi wamewahi kunyanyaswa kingono angalau mara moja, wakati asilimia 34.3 ya watoto wa shule kwa ujumla wamenyanyaswa  kisaikolojia hasa na wazazi au walezi.

‘Sisi sote kwa pamoja tunawajibu wa kutafuta ufumbuzi na kushughulikia sababu za unyanyasaji huu shuleni na nyumbani ili kuhakikisha watoto wanalelewa kwenye mazingira salama’..Amesema Dkt. Kalage

Kalage amesisitiza kuwa ili kufanikisha malengo yetu, inatupasa kwanza kuelewa maana au dhana ya ‘unyanyasaji/ukatili dhidi ya watoto’, dhana ambayo imekuwa na tafsiri tofauti kwenye jamii na kila mtu ana uelewa tofauti kutokana na misimamo yake ki dini, maadili, malezi au elimu yake.

Pia  ameisihi Serikali, pamoja na wadau wa elimu  na  mamlaka nyingine zote, kufikiria  kuwa na tafsiri moja ya dhana ya ukatili na unyanyasaji wa watoto, hali itakayosaidia kuwa na uelewa na msimamo wa pamoja kuhusu vitendo ambavyo tunakubaliana kuwa ni unyanyasaji wa watoto na namna ya kukabiliana navyo.

Sehemu ya mapendekezo ya HakiElimu kufuatia utafiti huo ni pamoja na kuangalia namna ya kuingiza kwenye mitaala ya vyuo vya ualimu mafunzo ya ulinzi wa mtoto na udhibiti  wa ukatili dhidi ya watoto ili walimu wanaohitimu wawe na uelewa huu utakaowalinda watoto.

Pia HakiElimu  inapendekeza kuwa Serikali  inapaswa ihakikishe kuwa shule zote zina wafanyakazi wenye ujuzi wa taaluma ya ushauri elekezi.

Mapendekezo mengine ni kuboresha Sheria na Sera zilizopo, hasa Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 sura ya 353 na marejeo ya mwaka 2002 na Kanuni za utoaji viboko shuleni – the Education (Corporal Punishment) Regulation G. N. 294 ya mwaka 2002 zinazozungumzia masuala mbalimbali ikiwemo adhabu za viboko shuleni.

Sheria inazitaka shule zote ziwe na Kanuni ya Nidhamu, lakini kwa bahati mbaya wakati wa kukusanya taarifa ya utafiti huu shule nyingi zilibainika kutokuwa na kanuni hizo, pamoja na kwamba walikuwepo walimu wa nidhamu. Ni matumaini yetu kuwa Kanuni hizi zitapendekeza na kusisitiza  adhabu mbadala au  nidhamu chanya, na zitatumika ipasavyo kwa matokeo chanya kwa wote.

Dkt. Kalage amehitimisha hotuba yake kwa kusema ni muhimu kuwa na jitihada za pamoja kuondoa vyanzo vya ukatili na unyanyasaji, kutoa taarifa na kuzifanyia kazi ipasavyo taarifa hizo, ili kufanikiwa kwenye lengo letu la kuona  watoto wa Tanzania wanatimiza ndoto zao  kwa kusoma na kuishi kwenye mazingira salama na rafiki kwao.