News

 Uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti Kuhusu Hali ya Upatikanaji wa Elimu Bora kwa Watoto Wanaoishi katika Makazi Duni na yasiyo rasmi Mijini.

Uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti Kuhusu Hali ya Upatikanaji wa Elimu Bora kwa Watoto Wanaoishi katika Makazi Duni na yasiyo rasmi Mijini.

Asasi ya Kiraia ya HakiElimu imezindua Ripoti ya Utafiti kuhusu hali ya upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wanaoishi katika Makazi duni na yasiyo rasmi, Mijini ambao unatarajia kusaidia kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto wanaoishi katika makazi duni nchini Tanzania.

Utafiti huo wa HakiElimu umefanywa kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Afrika ‘APHRC’, chenye makao yake makuu jijini Nairobi ambapo utafiti huo umefanyika mwaka 2022 katika mazingira duni ya mijini na umeifikia mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.

Akizungumza wakati akizindua ripoti hiyo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Mkurugenzi Uthibiti Ubora, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ndg. Ephraim Simbeye amesema mpango wa Maendeleo ya Sekta Elimu wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26 unagusia Elimu ya mjini.

“Mpango huu unatambua kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaohamia mijini kutoka vijijini hali ambayo imesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi mijini ukilinganisha na vijijini. Kutokana na hali hii, utafiti huu unatuimiza kuanza kuitumia dhana ya Elimu ya mjini katika mipango yetu”.

Ndugu Simbeye ametoa wito kwa HakiElimu na wadau wengine kuendelea kufanya tafiti na kuziwasilisha kwa umma kwani unatoa nafasi kwa wadau mbalimbali pamoja na Serikali kutumia matokeo yake katika kufanya maamuzi ambayo yanajengwa katika Ushahidi wa Kisayansi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt John Kalage amesema HakiElimu ilisukumwa kufanya utafiti huo kwa lengo la kupata hali halisi ya upatikanaji wa elimu katika maeneo ya mijini na kuikuza dhana ya elimu ya mjini “Urban Education” kama eneo la kitaaluma na utafiti.

“Mara zote inaelezwa kuwa shule za vijijini zina changamoto kubwa kuliko za mjini na haziwavutii walimu kutokana na usafiri mbaya na huduma duni za kijamii , Pia inaelezwa kuwa utendaji wa wanafunzi vijijini upo chini ukilinganisha na mijini. Hata hivyo, mtazamo huu si sahihi sana kwani shule za mijini pia zina wanafunzi wenye utendaji wa chini. Miji ina changamoto zake zinazofanana na za vijijini” alisema Dr. Kalage

Naye Mwakilishi wa Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Afrika ‘APHRC’ Ndugu Francis Kiroro ametaja sababu za uchaguzi wa maeneo yaliyofanyika utafiti huo “Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050, asilimia 55 ya watu Tanzania watakuwa mijini, huku Dar Es Salaam ikiongoza kwa ongezeko la watu mijini baraka Afrika, hivyo mipango madhubuti inahitajika”

Utafiti huu ulifanyika katika Jiji la Dodoma, kata ya Chang’ombe na Jiji la Dar-es-Salaam katika kata za Kipawa , kata ya Kiburugwa katika Manispaa ya Temeke na kata ya Hananasifu Manispaa ya Kinondoni, amedokeza Ndugu Francis Kiroro.