Marafiki wa Elimu wilayani Mpwapwa chini ya uratibu wa shirika la HakiElimu wamefanya uwasilishaji wa ripoti ya ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2022-2026. Ufuatiliaji huu ulilenga kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa Mkakati wa Elimu Jumuishi katika wilaya ya Mpwapwa kuanzia mwaka 2022 hadi 2024 katika ngazi ya shule na kwamba ulifanyika katika shule 15 za msingi za Idilo, Vingh’awe, Igovu, Kisokwe, Mazae, Ilolo, Ng’onje, Kikombo, Mpwapwa, Chazungwa, Mungui, Pwaga, Idaho, Makutupa, Magungu na shule 5 za sekondari za Ihala, Mount Igovu, Mwanakyanga, Pwaga na Vingh’awe.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa uwasilishaji wa ripoti hii, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ndugu Oberty Mwalyego amesema kipindi cha nyuma ilikuwa ni kawaida kusikia watoto wenye ulemavu wakifichwa majumbani na kunyimwa haki yao ya kupata elimu, ila kwasasa hali hiyo imebadilika sana na kwamba sasa watoto wenye ulemavu wanaandikishwa kwa wingi katika wilaya ya Mpwapwa na kutolea mfano wa uandikishaji katika shule ya Msingi Chazungwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Marafiki Elimu Mpwapwa ndugu Steven Noel akiwasilisha matokeo hayo alisema wamebaini ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka wanafunzi 196 (wasichana 127 na wavulana 69) kwa mwaka 2022 hadi wanafunzi 1,022 (wasichana 392 na wavulana 630) kwa mwaka 2024; na wanafunzi wenye ulemavu kutoka wanafunzi 25 (wasichana 12 na wavulana 13) kwa mwaka 2022 hadi wanafunzi 68 (wasichana 27 na wavulana 41) kwa mwaka 2024.
Akitoa ushuhuda wa namna ambavyo alipata fursa ya elimu, ndugu Kandido Mnemele mwakilishi wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Mpwapwa (SHIVYAWAPWA) anasema ‘’Nakumbuka siku moja nilikuwa nacheza na rafiki zangu ambao walikuwa wamevaa sare za shule na Mwalimu mmoja alipita pale tulipokuwa tunacheza alishangaa kwanini mimi sikuwa nimevaa sare, yule Mwalimu alisimama na kuniuliza kwanini nilikuwa sijaandikishwa shuleni na akanitaka kesho yake niende shuleni kuandikishwa’’
Ushuhuda wa Kandido unaonesha namna ambavyo Walimu wanayo nafasi adhimu ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu na wao wapate fursa ya elimu kama watoto wengine ‘’hii confidence mnayoniona nayo leo ni kwasababu Walimu walinionesha upendo, ni muhimu kuwa na watu ambao watatembea kwenye jamii na kuwatambua watoto wenye ulemavu na kuwaandikisha, Mimi pia nilitambuliwa hivyo’. aliongeza ndugu Kandido.
Akihitimisha mkutano huo wa wadau, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ndugu Oberty Mwalyego alisema ‘’Kuvaa dera sio kazi bali kazi ni kulishikilia, hivyo natoa wito kwa wadau wa elimu na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa watoto wote wenye ulemavu wanaoandishwa shuleni wanaendelea kujifunza katika mazingira wezeshi ili wafikie malengo yao ya kielimu lakini pia kuzifikia ndoto zao’’.