News

The State of Violence against School Children in Mainland Tanzania Report Launching

Hali ya Ukatili dhidi ya Watoto wa Shule Tanzania Bara’, ambao  umefanyika mwaka 2019.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalage wakati wa uzinduzi  wa Utafiti  huo jijini Dar es salaam amesema dhumuni kuu la Utafiti huo lilikuwa ni kupata taarifa rasmi na kujifunza hali halisi kuhusu ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto shuleni, pamoja na kuelewa vyanzo vya ukatili huo na kuboresha ulinzi na usalama wa watoto walio shuleni Tanzania Bara.

Utafiti huo umefanyika kwenye Wilaya 32 za  Tanzania Bara na kuzifikia shule 128, na unaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu kwenye mazingira salama shuleni na nje ya shule, hususani Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Unyanyasaji wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) (2017/18 – 2021/22).

Matokeo ya utafiti yameonyesha uwepo mkubwa wa matukio ya unyanyasaji wa watoto katika mifumo tofauti. Na takribani asilimia 87.9 ya watoto wote walio sailiwa, wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili ( physical violence), hususani kupitia adhabu za viboko.

Pia Utafiti umeonyesha kuwa asilimia 17.0 ya watoto walio shule za umma na asilimia 14.3 walio shule binafsi wamewahi kunyanyaswa kingono angalau mara moja, wakati asilimia 34.3 ya watoto wa shule kwa ujumla wamenyanyaswa  kisaikolojia hasa na wazazi au walezi.

‘Sisi sote kwa pamoja tunawajibu wa kutafuta ufumbuzi na kushughulikia sababu za unyanyasaji huu shuleni na nyumbani ili kuhakikisha watoto wanalelewa kwenye mazingira salama’..Amesema Dkt. Kalage

Kalage amesisitiza kuwa ili kufanikisha malengo yetu, inatupasa kwanza kuelewa maana au dhana ya ‘unyanyasaji/ukatili dhidi ya watoto’, dhana ambayo imekuwa na tafsiri tofauti kwenye jamii na kila mtu ana uelewa tofauti kutokana na misimamo yake ki dini, maadili, malezi au elimu yake.

Pia  ameisihi Serikali, pamoja na wadau wa elimu  na  mamlaka nyingine zote, kufikiria  kuwa na tafsiri moja ya dhana ya ukatili na unyanyasaji wa watoto, hali itakayosaidia kuwa na uelewa na msimamo wa pamoja kuhusu vitendo ambavyo tunakubaliana kuwa ni unyanyasaji wa watoto na namna ya kukabiliana navyo.

Sehemu ya mapendekezo ya HakiElimu kufuatia utafiti huo ni pamoja na kuangalia namna ya kuingiza kwenye mitaala ya vyuo vya ualimu mafunzo ya ulinzi wa mtoto na udhibiti  wa ukatili dhidi ya watoto ili walimu wanaohitimu wawe na uelewa huu utakaowalinda watoto.

Pia HakiElimu  inapendekeza kuwa Serikali  inapaswa ihakikishe kuwa shule zote zina wafanyakazi wenye ujuzi wa taaluma ya ushauri elekezi.

Mapendekezo mengine ni kuboresha Sheria na Sera zilizopo, hasa Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 sura ya 353 na marejeo ya mwaka 2002 na Kanuni za utoaji viboko shuleni – the Education (Corporal Punishment) Regulation G. N. 294 ya mwaka 2002 zinazozungumzia masuala mbalimbali ikiwemo adhabu za viboko shuleni.

Sheria inazitaka shule zote ziwe na Kanuni ya Nidhamu, lakini kwa bahati mbaya wakati wa kukusanya taarifa ya utafiti huu shule nyingi zilibainika kutokuwa na kanuni hizo, pamoja na kwamba walikuwepo walimu wa nidhamu. Ni matumaini yetu kuwa Kanuni hizi zitapendekeza na kusisitiza  adhabu mbadala au  nidhamu chanya, na zitatumika ipasavyo kwa matokeo chanya kwa wote.

Dkt. Kalage amehitimisha hotuba yake kwa kusema ni muhimu kuwa na jitihada za pamoja kuondoa vyanzo vya ukatili na unyanyasaji, kutoa taarifa na kuzifanyia kazi ipasavyo taarifa hizo, ili kufanikiwa kwenye lengo letu la kuona  watoto wa Tanzania wanatimiza ndoto zao  kwa kusoma na kuishi kwenye mazingira salama na rafiki kwao.