Jumatano, Oktoba 01, 2025
Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (National Safe School Coalition - NSSC) ni mtandao wa mashirika zaidi ya 20 ya Kiraia (CSOs) uliozinduliwa Machi 2024, unaofanya kazi Tanzania Bara na Visiwani. Umoja huu umejikita katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama ya kujifunzia na kukua bila ukatili, kwa kuhimiza jamii isiyokubali adhabu za viboko na aina zote za ukatili ndani na nje ya shule.
Kwa kutambua kuwa Taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025, sisi Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NSSC) tukishirikiana na wadau wa vyombo vya habari wanaojihusisha na elimu ya uraia na ustawi wa watoto, tunatoa wito huu wa dharura. Ni rai yetu ya pamoja kuwa usalama na ulinzi wa watoto lazima viwe kipaumbele katika kipindi chote cha uchaguzi.
Watoto Wapo Katika Hatari Kubwa Katika Vipindi vya Uchaguzi.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Watoto Na. 6 ya 2011 ya Zanzibar zinafafanua kuwa mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18. Watoto wamekuwa miongoni mwa makundi yaliyo hatarini zaidi – kutokana na ama kuachwa bila uangalizi huku wazazi na walezi wakijihusisha na shughuli za uchaguzi au kutumika vibaya katika shughuli za kisiasa na kampeni.
Kipindi hiki pia huwaweka watoto katika hatari kubwa zaidi kutokana na mila potofu, ikiwa ni pamoja na imani za kishirikina. Watoto wenye ulemavu hasa wenye ualbino wamekuwa wakikumbana na ukatili mkubwa katika vipindi vya uchaguzi. Ukatili huu huleta hofu, mazingira yasiyo salama, athari za kisaikolojia, maumivu na hata vifo kwa watoto na familia zao.
Wito Muhimu wa Kuchukua ili kuwalinda Watoto
Kwa kuzingatia hali hii, sisi wanachama wa Umoja huu tunatoa wito ufuatao:
- Mashirika ya Kiraia (AZAKI) na NGOs
Endeleeni kutoa elimu ya uraia na ya mpiga kura inayojumuisha ujumbe wa kulinda haki za watoto katika kampeni zote za elimu ya uraia. AZAKI na NGOs zitoe kipaumbele katika kuhamasisha umma kuhusu hatari maalum zinazowakabili watoto wakati wa uchaguzi mkuu. Ni wajibu wao kuripoti na kutunza kumbukumbu za ukiukwaji haki dhidi ya watoto, na kushirikiana na jamii ili kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia na wa dharura inapohitajika ili kumlinda mtoto.
- Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii
Toeni nafasi kwa sauti za watoto kwenye taarifa zenu na mijadala ya umma. Hakikisheni mnaepuka lugha au ujumbe unaoweza kueneza chuki dhidi ya watoto na jamii. Vyombo vya habari vina wajibu wa moja kwa moja wa kuendeleza mijadala ya kisiasa inayomlinda mtoto. Pia vihakikishe vinatoa majukwaa ya kuripoti kwa maadili na kushughulikia matukio ya ukatili dhidi ya watoto. Vyombo vya habari pia vitoe taarifa na kuhabarisha umma juu ya vyama, wagombea au taasisi zinazowatumia vibaya Watoto katika kipindi hiki, ikiwa ni pamoja na kuwanyima haki yao ya kujifunza kwa kuwatoa darasani ili wahudhulie mikutano ya kampeni.
- Vyama vya Siasa na Wagombea
Toeni kipaumbele juu ya haki na mahitaji ya watoto katika kampeni zenu. Tunahimiza kila chama na mgombea kutoa mpango wao wa kulinda na kuhudumia haki za watoto kabla na baada ya uchaguzi, bila kujali matokeo ya ushindi au kushindwa. Masuala kama upatikanaji wa elimu bora, huduma za afya, ulinzi dhidi ya ukatili na ustawi wa kijamii yazingatiwe kwenye ilani na mipango yao kabla na baada ya kampeni. Ni wajibu wa wanasiasa kuheshimu haki za watoto na waepuke kuwatumia au kuwahusisha watoto kwenye shughuli za kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuwasafirisha kutoka eneo moja hadi jingine kwa ajili ya mikutano ya kampeni.
- Wazazi na Jamii
Wahakikishe usalama wa watoto hususani karibu na vituo vya kupigia kura, mikutano ya kampeni na mikusanyiko ya umma. Wazazi na jamii wana wajibu wa kuripoti matukio yoyote ya ukatili au vitisho dhidi ya watoto na kudai uwajibikaji katika kuheshimu haki za watoto wakati na baada ya uchaguzi. Kama wapiga kura, wazazi na jamii wawahoji wagombea kuhusu mipango yao ya kulinda watoto. Tunawahimiza wapiga kura wote kuwaeleza wagombea kwamba kura zao zinahusiana na dhamira ya kulinda watoto.
- Kwa Serikali na Taasisi Zake (Polisi, Vyombo vya Usalama, Serikali za Mitaa na Kuu):
Wachukue hatua za mapema kuhakikisha usalama wa watoto wakati wa uchaguzi, hususan karibu na vituo vya kupigia kura, mikutano ya kampeni na mikusanyiko ya umma. Taasisi hizi zina jukumu la kuitikia haraka ukiukwaji wowote dhidi ya watoto na kutoa huduma za ulinzi na msaada zinazohitajika.
Mtoto Si Mgombea wala Mpiga Kura
Ikumbukwe kuwa, Mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 haruhusiwi kisheria kushiriki uchaguzi Mkuu kwa namna yoyote iwe ya kupiga kura au kugombea. Kwa muktadha huu, hatutegemei kwa namna yoyote kumuona mtoto akishiriki katika kampeni au mikutano ya kisiasa kwaajili ya kampeni za uchaguzi huu Mkuu. Ni wajibu basi wa vyombo hivi kuwakumbusha na kuwasimamia wanachama au vyama vya kisaisa ambavyo kwa namna moja ama nyingine wanakiuka haki hii ya msingi ya kikatiba kwa Watoto.
Sisi wanachama wa Umoja wa Shule Salama tunatoa wito kuwa uchaguzi huu uwe alama ya uzingatiwaji wa haki za jamii na hususani Watoto. Suala la ulinzi na usalama wa mtoto ni suala la kitaifa linalovuka mipaka ya itikadi zetu za vyama, ni suala la ulinzi wa taifa la kesho na hivyo ni muhimu kuwa na nia moja na wivu mkubwa kulinda tabaka hili la Watoto na taifa la kesho. Watoto wanastahili kukua kwa amani, bila hofu na wakiwa wamezungukwa na watu wazima wanaolinda haki zao. Tunatoa rai kwa wananchi wote kuwa macho, wenye huruma na kuchukua hatua kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa kwenye hatari wakati huu muhimu wa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Umetayarishwa na kutolewa na wanachama wa Umoja huu:
Kaya Foundation, HakiElimu, Save the Children, SAWA Morogoro, MTWANGONET, Msichana Initiative, ZAFELA, TAMWA, ZALHO, WILDAF, My LEGACY, CDF, Child Support Tanzania, HGWT, ZCRF, TCRF, ZAPHA+, Children in Cross Fire, Amani Girls Organization, Women Fund Tanzania Trust, Shule Direct, TENMET & CAMFED.