News & Events

Shule zinapaswa kuwa mahali Salama kwa Watoto Kujifunza

Shule zinapaswa kuwa mahali Salama kwa Watoto Kujifunza

HakiElimu, ikishirikiana na Kikosi Kazi cha Kupinga Adhabu ya Viboko Shuleni, imepokea kwa masikitiko mkubwa taarifa za kifo cha mwanafunzi Peter Maira, aliyekuwa akisoma kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Makongoro, iliyopo Wilayani Bunda, Mkoa wa Mara.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari, mwanafunzi huyo anadaiwa kupewa adhabu ya viboko shuleni, akapata matatizo ya kiafya na baadaye kufariki dunia akiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Taarifa hizo pia zinaeleza kuwa Jeshi la Polisi limeshaanza uchunguzi wa tukio hilo.

Msimamo na Wito Wetu:

  • Uchunguzi Huru na wa Kina: Tunaliomba Jeshi la Polisi na mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka, huru, na wa wazi ili kubaini chanzo halisi cha kifo hicho na kuhakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.
  • Uzingatiaji wa Sheria: Mfumo wa kisheria nchini—ikiwemo Education (Corporal Punishment) Regulations, 2002 na Sheria ya Mtoto (Law of the Child Act, 2009 [R.E. 2023]) — unataka adhabu yoyote shuleni iwe ya kiasi, isizidi viboko vinne, na ilinde utu pamoja na afya ya mtoto.
  • Usimamizi wa Nidhamu Chanya: Tunazihimiza mamlaka za elimu na shule zote nchini kuimarisha matumizi ya Nidhamu Chanya (Positive Discipline) na ushauri nasaha badala ya adhabu za kimwili zinazoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

"Shule inapaswa kuwa mahali salama kwa kila mtoto kujifunza, kukua, na kutimiza ndoto zake bila hofu ya kupata madhara ya kimwili au kisaikolojia."

Ili kusoma na kupakua tamko kamili la Kikosi Kazi pamoja na msimamo wetu wa kina kuhusu tukio hili, tafadhali bofya kiungo hiki: 👉 Pakua Tamko Rasmi la Kikosi Kazi Hapa