News & Events

Malala Yousafzai Azuru HakiElimu: Aongoza Mjadala wa Wadau kuhusu elimu ya mtoto wa kike nchini Tanzania

Malala Yousafzai Azuru HakiElimu: Aongoza Mjadala wa Wadau kuhusu elimu ya mtoto wa kike nchini Tanzania

Julai 10, 2025, HakiElimu ilipata heshima ya kipekee kutembelewa na Mwanaharakati maarufu kutoka nchini Pakistan na mshindi mwenye umri mdogo zaidi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai anayejulikana kwa kazi yake ya utetezi wa haki ya wasichana.

Akiwa HakiElimu, Malala ambaye aliambatana na ujumbe kutoka Malala Fund alipata wasaa wa kuongoza mjadala ulioangazia fursa na vikwazo dhidi ya mtoto wa kike ukihusisha washiriki kutoka mashirika manne yanayofadhiliwa na Malala Fund ambayo ni HakiElimu, Msichana Initiative, Hope 4 Young Girls, na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET).

Ziara ya Malala katika ofisi za HakiElimu ni hatua muhimu ya ushirikiano unaoendelea kati ya shirika la HakiElimu na Malala Fund, ushirikiano ambao unalenga kuendeleza elimu ya wasichana nchini Tanzania. Kupitia ushirikiano huu, HakiElimu kwa sasa inatekeleza mradi ujulikanao kama Education Champion Network (ECN) mradi unaolenga kuboresha mazingira jumuishi ya ujifunzaji, na salama kwa wasichana katika shule 60 zilizoko kwenye wilaya 11 za Muleba, Mpwapwa, Kigoma, Njombe, Mbeya, Kilosa, Manispaa ya Tabora, Iramba, Musoma, Korogwe, na Moshi.

Mradi wa ECN unawanufaisha moja kwa moja wanafunzi 11,772 (wasichana 8,116 na wavulana 3,656) kupitia afua zinazolenga kuboresha matokeo ya kielimu na kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika safari ya elimu.

Kupitia mradi huu HakiElimu inafanya kazi ya utetezi wa sera na uzalishaji wa tafiti zitakazosaidia kufanya maamuzi ya kisera sambamba na hili pia unalenga kuimarisha uwezo wa mamlaka za serikali za mitaa na uongozi wa shule katika kuzuia ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na kupinga mila na desturi zenye madhara hasi kwa wasichana ili kuwawezesha wasichana waliotengwa kijamii kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao za kielimu.