News & Events

HakiElimu Yazindua Kampeni ya Kitaifa ya “Tuwatambue Mapema, Tuwasaidie Vema” Kuimarisha Huduma za Utambuzi na Upimaji wa Awali kwa Watoto

HakiElimu Yazindua Kampeni ya Kitaifa ya “Tuwatambue Mapema, Tuwasaidie Vema” Kuimarisha Huduma za Utambuzi na Upimaji wa Awali kwa Watoto

Mbeya, Tanzania

Shirika la HakiElimu limezindua kampeni maalum ya kitaifa yenye lengo la kuhamasisha ujenzi, uboreshaji na matumizi ya Vituo vya Utambuzi na Upimaji wa Awali kwa Watoto (ESRACs), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za utambuzi wa mapema kwa watoto wenye mahitaji mbalimbali ya ujifunzaji na maendeleo.

Kampeni hiyo, yenye kaulimbiu “Tuwatambue Mapema, Tuwasaidie Vema,” imezinduliwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, na imeandaliwa na HakiElimu kwa ushirikiano na Child Support Tanzania (CST).

Umuhimu wa huduma hizi unaonekana wazi kupitia takwimu za Kituo cha ESRAC cha shule ya Msingi Mwenge, ambapo katika kipindi cha Januari hadi Mei 2026 pekee, watoto 203 walipatiwa huduma za upimaji na utambuzi wa awali, wakiwemo wavulana 143 na wasichana 60. Mwaka 2025, kituo hicho kilitoa huduma kwa watoto 199, wakiwemo wavulana 141 na wasichana 58. Takwimu hizi zinaonesha ongezeko la mahitaji ya huduma za utambuzi wa mapema na umuhimu wake katika kuwawezesha watoto kupata msaada stahiki kwa wakati.

Wito kwa Halmashauri Kuimarisha Huduma za Utambuzi wa Awali

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mhe. Brigedia Jenerali Maulid Hassan Surumbu, ametoa wito kwa viongozi wa halmashauri nchini kuhakikisha kuwa vituo vya utambuzi na upimaji wa awali vinapatikana katika maeneo yao ili kila mtoto aweze kupata elimu inayozingatia mahitaji yake binafsi.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika huduma za utambuzi wa mapema ni msingi muhimu wa kujenga mfumo wa elimu jumuishi unaowezesha watoto wote kupata fursa sawa za kujifunza na kufanikiwa, bila kujali changamoto wanazokabiliana nazo.

Utambuzi wa Mapema ni Mlango wa Fursa kwa Watoto

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Mary Ndaro, amesema kuwa vituo vya ESRACs vina mchango mkubwa katika kubaini mahitaji ya watoto mapema na kuwaunganisha na huduma stahiki za elimu na maendeleo.

"Tunaposimama hapa leo, tunaona zaidi ya jengo au vifaa vya upimaji. Tunaona watoto ambao leo wanapata nafasi ya kutambuliwa mapema na kupata msaada wanaouhitaji ili waweze kujifunza na kushiriki kikamilifu katika elimu kama watoto wengine. Tunaona matumaini mapya kwa wazazi na walimu," amesema Bi. Ndaro.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa utambuzi na upimaji wa mapema na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika huduma zinazowawezesha watoto kufikia uwezo wao kamili.

Kwa Nini Utambuzi wa Mapema ni Muhimu?

Naye Mkurugenzi wa Child Support Tanzania (CST), Bi. Noelah Godfrey Msuya, amesema kuwa utambuzi wa mapema huwasaidia walimu, wazazi na wataalamu kuelewa mahitaji halisi ya mtoto na kubaini mbinu sahihi za kumsaidia katika mazingira ya kujifunzia.

Akifafanua zaidi, Bi. Msuya ametolea mfano changamoto ya dyscalculia — hali inayosababisha ugumu wa kujifunza hesabu. Amesema watoto wengi wenye changamoto hiyo mara nyingi huonekana kuwa wavivu au wasiopenda kujifunza somo la hesabu, ilhali ukweli ni kwamba wanahitaji tathmini ya mapema na mbinu maalumu za ufundishaji.

"Mimi ni miongoni mwa watoto wa wakati huo ambao hawakufanyiwa upimaji mapema," amesema Msuya. "Huenda walimu wangu hawakugundua kuwa nilikuwa na changamoto ya dyscalculia."

Uzoefu wake binafsi unaonesha umuhimu wa kuwabaini watoto mapema ili wapate msaada wanaouhitaji kwa wakati ili kuwawezesha kufanikiwa katika elimu na maisha yao ya sasa na baadaye.

Ushuhuda wa Mzazi: “Utambuzi Umenipa Matumaini”

Bi. Angela Charles, mmoja wa wazazi wenye mtoto mwenye mahitaji maalumu, alitoa ushuhuda wake kuhusu manufaa ya utambuzi wa mapema.

Alieleza kuwa kwa muda mrefu hakuwa akifahamu chanzo cha changamoto zilizokuwa zikimkabili mtoto wake. Hata hivyo, baada ya mtoto kufanyiwa tathmini, alipata mwongozo sahihi wa namna ya kumsaidia na kumwezesha kupata mazingira bora ya kujifunzia.

"Mtoto wangu ana ulemavu wa akili. Awali sikuwa naelewa kabisa tatizo lake, lakini baada ya kupata utambuzi nilielekezwa namna ya kumsaidia na kumpeleka katika shule hii ya Child Support," amesema.

Ushuhuda huo unaonesha namna huduma za utambuzi wa awali zinavyoweza kubadilisha maisha ya watoto na familia zao kwa kuwapa maarifa, msaada na matumaini mapya.

Hali Halisi ya Vituo vya ESRACs Nchini

Pamoja na umuhimu mkubwa wa vituo vya ESRACs, takwimu zinaonesha kuwa bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma hizo nchini.

Ikiwa ni takribani miaka 5 imepita tangu serikali ilipotoa mwongozo wa uanzishwaji a vituo hivi katika ngazi ya halmashauri zote nchini mwaka 2022, takwimu zinaonesha kuwa kati ya halmashauri 184 zilizopo Tanzania, ni halmashauri 36 pekee zenye vituo vya ESRACs. Aidha, vituo vingi vilivyopo bado vinakabiliwa na changamoto za miundombinu, upungufu wa vifaa muhimu pamoja na uhaba wa wataalamu wenye ujuzi wa kutoa huduma hizo.

Kutokana na hali hiyo, watoto wengi wanaendelea kuchelewa kutambuliwa na kupata huduma wanazohitaji. Wengine hushindwa kueleweka darasani na kuonekana kama wavivu au wasiotaka kujifunza, wakati ukweli ni kwamba wanahitaji tathmini na msaada wa kitaalamu ili kufikia uwezo wao wa kujifunza.

Wito wa Pamoja kwa Jamii na Wadau wa Elimu

Uzinduzi wa kampeni ya “Tuwatambue Mapema, Tuwasaidie Vema” ni wito kwa jamii, wadau wa elimu, sekta binafsi na serikali kushirikiana kuhakikisha upatikanaji wa vituo vya ESRACs katika kila halmashauri nchini.

Kupitia kampeni hii, HakiElimu na washirika wake wanakusudia kuhamasisha uwekezaji zaidi katika huduma za utambuzi wa mapema ili kuhakikisha kila mtoto anatambuliwa kwa wakati, anapata msaada stahiki na anapewa fursa sawa ya kujifunza, kushiriki na kufanikiwa.

Kwa pamoja, tunaweza kujenga mfumo wa elimu jumuishi unaomfikia kila mtoto na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.