skip to Main Content
+255754 354681 info@hakielimu.or.tz

Wiki ya AZAKi 2021

HakiElimu katika maadhimisho ya Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKi) 2021, Dodoma.

Wiki ya AZAKI ni tukio la kila mwaka lililoanzishwa rasmi mwaka 2018, linaloandaliwa na muungano wa asasi za Kiraia kutoka  ndani na nje ya Tanzania. Lengo kuu la Wiki ya  AZAKi ni kuimarisha mahusiano miongoni mwa wadau mahususi wa maendeleo. Wiki ya AZAKi kwa mwaka 2021 ilifanyika katika kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini  Dodoma ambapo kauli mbiu kwa mwaka huu ilikuwa ni “Mchango wa AZAKi kwa Maendelao ya Taifa.”

Shirika la HakiElimu likiwa mojawapo ya Asasi za Kiraia hapa nchini ambalo limejikita zaidi katika kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, lilipata fursa ya kushiriki katika maadhimisho hayo kwa kuonyesha kazi mbalimbali zinazofanywa na shirika, sambamba na kushiriki kwenye mkutano mkuu. Mgeni rasmi katika maonyesho haya alikuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ngugai mbaye katika wasilisho lake alikiri kuwa serikali inatambua mchango mkubwa unaotokana na kazi mbalimbali zinazofanywa na AZAKi.

HakiElimu ilitumia fursa hii kusambaza machapisho mbalimbali ambayo yana taarifa za msingi  na zilizofanyiwa utafiti wa kina kuhusu masuala mbalimbali ya elimu. Sambamba na machapisho,shirika lilitumia fursa hii kuonyesha mubashara matangazo mbalimbali ambayo hasa yanalenga kuchochea mjadala kuhusu elimu kwa watoto wa kike na motisha kwa walimu.Watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania walitembelea banda la HakiElimu kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusu kazi za shirika.Wengine walifika kwa lengo la kupongeza kazi nzuri zinazofanywa na HakiElimu huku wakitamka wazi kuwa, kazi hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuibua mjadala kuanzia ngazi ya wananchi mpaka serikalini, hivyo kuchagiza mabadiliko chanya  na maendeleo katika sekta ya elimu.

Aidha, mbali na kushiriki kwenye maonyesho ya kazi mbalimbali, Mkurugezni Mtendaji wa Shirika la HakiElimu Dkt.John Kalage akiongozana na Meneja wa Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera Ndugu Mwemezi Makumba walishiriki katika mkutano mkuu ambao uliwakusanya viongozi wakuu wa Asasi za Kirai, wawakilishi kutoka wizara na taasisi  mbalimbali za serikali  pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania. Mkutano huu ulilenga kuwasilisha mada mbalimbali kutoka kwa wawakilisha wa Asasi za Kiraia ambapo shirika la HakiElimu lilipata fursa ya kuchangia  mada kuu mbili. Mada ya kwanza ilihusu  ‘Mchango wa Asasi za Kiraia kwenye uchumi wa Tanzania’ na ya pili iliangazia ‘Kama mifumo na mbinu zilizopo zinawezesha ushiriki wa wananhi katika mchakato wa sera na bajeti’, ambapo katika mada hii ya pili Makumba Mwemezi alipata fursa ya kuwa mmojawapo wa wazungumzaji na alitilia mkazo kuwa, ushirikiano ulioimarishwa kati ya AZAKi na serikali utaongeza ushiriki wa wanachi katika mchakato wa sera na bajeti.

Back To Top