skip to Main Content
+255754 354681 info@hakielimu.or.tz

HakiElimu yakamilisha Mradi wa Uwajibikaji kwa mtoto wa kike kwa kishindo

Na Mwandishi wetu

Mradi wa AGE (Accountability for Girls Education) yaani uwajibikaji kwa Elimu ya mtoto wa kike, ulioanza kutekelezwa mwaka 2021 umekamilishwa kwa kishindo April mosi 2022 kwenye wilaya 5 za Tanzania Bara ambazo ni Mpwapwa, Iramba, Tabora Manispaa, Kigoma vijijini na Korogwe.

Mradi huo ulianza kutekelezwa baada ya HakiElimu kupata fungu maalumu kutoka Ufadhili wa Serikali ya Uingereza kwaajili ya kuonyesha kwa vitendo namna gani mazingira ya Elimu kwa mtoto wa kike yanapaswa kuwa.

Mradi ulikuja kwa muda muafaka kwa kuzingatia takwimu zilizoonyesha kuwa takribani watoto 6000 wanaacha shule kutokana na sababu za ujauzito kila mwaka huku wasichana wengi wakipoteza siku takribani 5 kila mwezi kwa sababu ya hedhi.

Takwimu za Serikali na taarifa mbalimbali za Elimu zinaonyesha kuwa umbali mrefu, ukosefu wa mabweni pamoja na ukosefu wa vyoo bora shuleni imekuwa changamoto kubwa kwa wasichana, hali iliyotajwa kuwakanyaga watoto wa kike katika safari yao ya kielimu kwenye Wilaya zote ambazo mradi huo ulizifikia.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalage alipotembelea Miradi ya vyoo, maji na mabweni kwenye Wilaya tajwa alisema:

 “Changamoto zilizozikumba Wilaya hizi, Uwajibikaji na Ushirikiano mzuri kutoka kwa Viongozi wa Halmashauri za Wilaya ambazo zilifikiwa, jitihada za Marafiki wa Elimu na Wananchi ni sababu kubwa zilizoifanya HakiElimu kutekeleza mradi huu kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

“Tuliamua kuonyesha kwa vitendo namna #ElimuTunayoitaka inapaswa kuwa na ni mazingira gani tunahitaji yawekwe kwenye shule ili kupunguza mdondoko kwa watoto wa kike, kwa hiyo licha ya masuala ya kisera ambayo tunayamulika pamoja na kufanya tafiti mbalimbali tuliona tuwashike mkono wanajamii ambao wameshiriki kwa ufanisi kuhakikisha wanazimulika changamoto, kupaza sauti na kuanzisha jitihada ambazo zimefanyika na HakiElimu ikaunga mkono jitihada hizo ” alisema Dkt. Kalage.

Dkt. Kalage aliongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa wasichana wengi wanaandikishwa kuanza shule lakini kutokana na changamoto nyingi zikiwemo umbali mrefu, ukosefu wa mabweni pamoja na ukosefu wa vyoo bora, huwafanya wasichana kukumbwa na mdondoko kwenye safari ya Elimu.

Je, Nini kimefanyika kwenye Wilaya hizo 5?

Mpwapwa – Dodoma

Katika kukabiliana na Changamoto ya Maji kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Idilo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma @HakiElimu kwa kushirikiana na wananchi wamekamilisha Mradi wa Maji uliogharimu takribani Tsh. Milioni 26.

Mradi huo umezinduliwa Jumatatu Machi 21, na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpwapwa Mhe. William Madanya, akiambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalage, Walimu, Wananchi pamoja na watendaji wengine wa Wilayaya Mpwapwa.

Kabla ya Mradi huo kukamilika wanafunzi walilazimika kuyafuata Maji umbali mrefu huku baadhi ya wasichana wakishindwa kuhudhuria masomo wanapokuwa kwenye hedhi.

Mradi huo pia utawasaidia Wananchi ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri Ndugu William Madanya ameagiza wananchi kuchangia kiasi kidogo cha pesa kila wanapochota maji ili pesa hizo zisaidie uendeshaji wa mradi huo na mahitaji mengine ya shule.

Vilevile mradi wa AGE umefanikisha ujenzi wa Choo bora na cha kisasa kwa wasichana katika shule ya Sekondari Ving’hawe, choo kina matundu 8 na chumba maalumu kwaajili ya kujisitiri watoto wa kike wawapo kwenye siku za hedhi. Choo kimegharimu takribani Tsh. Mlioni 22.

Iramba – Singida

Vyoo viwili vya kisasa kwaajili ya watoto wa kike vimejengwa kwa nguvu za wananchi na HakiElimu kwenye shule za Sekondari New Kiomboi na shule ya Sekondari Mgongo. 

Vyoo hivyo vina matundu 13 kila kimoja na vina vyumba maalumu kwaajili ya wasichana kujisitiri wakati wa hedhi sanjari na choo maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu.

Vyoo vya shule hizo mbili za Iramba vimejengewa sehemu ya kuchoma sodo ‘incinerator’ ambapo msichana akiwa kwenye chumba maalumu kuna kidirisha kidogo kwaajili ya kutupa sodo ambako itachomewa moto bila kuonekana na watu wengine. 

Choo cha Shule ya Sekondari Mgongo kimegharimu Tsh. Milioni 26 huku Choo cha shule ya Sekondari New Kiomboi kikigharimu Tsh. Milioni 25.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba Sando Pius Songoma alimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo kuzindua miradi hiyo miwili ambapo pamoja na mambo mengine alisema takribani watoto watatu mpaka saba huripotiwa kupata ujauzito kila mwezi wilayani Iramba kutokana na changamoto za umbali na ukosefu wa usimamizi mzuri wa watoto wa kike wilayani humo. 

“Mimi ninawashukuru sana wadau wetu HakiElimu, Iramba bado tunawahitaji sana, msitusahau tuna shida, kwa sekondari tuna shule 23 na Wilaya yetu ina changamoto nyingi. Watoto wanatoka mbali na maeneo ya shule, ukipita Maluga mpaka Malendi kueleka shule kama Kizaga mpaka Shelui na nyingine, muda wote utawaona wanafunzi wanasimamisha magari kupata lifti” alisema Songoma.

“Matokeo ya zile lifti yanakatisha ndoto zao, matokeo ni tunaendelea kuwa masikini, ndoto za watoto wa kike zinakatishwa, anajifungua hana uwezo wa kulea, aliyempa ujauzito anakimbia mzunguko wa umasikini unaendela kuwepo” DAS huyu wa Iramba.

Tabora Manispaa.

Uzinduzi wa kitaifa wa miradi yote chini ya AGE umefanyika Mkoani Tabora ambapo Mkuu wa Mkoa huu Dkt. Batilda Burian akiambatana na Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt John Kalage pamoja watendaji wengine wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya alifanya Uzinduzi wa miradi ya vyoo kwenye shule ya msingi Kazima, Shule ya Msingi Isike, Shule ya Sekondari Fundikira na Bweni la wasichana kwenye shule ya Sekondari Itonjanda. Miradi yote iligharimu Tsh. Milioni 150.

Hosteli iliyojengwa kwenye shule ya sekondari Itonjanda ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 na itasaidia kwa kiwango kikubwa wasichana kupata muda mwingi wa kusoma wakiwa shuleni na kuepuka kutembea umbali mrefu ambapo walikabiliwa na vishawishi vingi vya wanaume wawapo njiani.

Katika uzinduzi huo Dkt. Batilda Burian alisema jitihada za ujenzi wa hosteli zinaendana na juhudi za serikali za kuhakisha wasichana wanasoma kwenye mazingira rafiki.

Vile vile Mkuu huyo wa Mkoa alisema licha ya uamuzi wa Serikali kuwaruhusu wanafunzi waliopata mimba kurejea shuleni baada ya kujifungua, bado zinahitajika jitihada za kupambana na ngono kwa wanafunzi, ndoa pamoja na mimba za utotoni na mahusiano ayanayokwenda kinyume na maadili na utamaduni wa Kitanzania.

“Serikali kupitia Rais wetu Samia Suluhu Hassan haijahalalisha wanafunzi wajiingize kwenye mahusiano na kupata mimba na kurejea shuleni , bali lengo ni kuwapa nafasi waliopitia changamoto hiyo ili wapate Haki ya Elimu”.

Akizungumzia jitihada za wadau kwenye kuondoa vikwazo ili watoto wasome, Mkuu huyo wa Mkoa alisema HakiElimu imekuwa msaada mkubwa kwenye kuinua elimu Mkoani Tabora na miradi aliyoizindua itakua chachu ya kupunguza mdondoko na kuinua kiwango cha Elimu mkoani mwake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalage alisema:

“Tuliamua kwamba tunahitaji kuwa na maeneo ambayo tutawekeza nguvu za ziada kushirikiana na wananchi na serikali, na sisi pamoja na tafiti na kufanya ushawishi wa sera, tuna wajibu wa kuwashika mikono na kuleta mabadiliko na tukajifunza kwa pamoja.

“Kwa bahati nzuri Tabora ina shule 8 kati ya shule hizo 127 tunazofanya nazo kazi, nilichokiona leo ni mwitikio na ushirikiano mkubwa baina ya Serikali na wananchi na ndio maana kila inapotokea fursa lazima tuikumbuke Tabora” alihitimisha Dkt.Kalage.

Katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt Yahya Nawanda aliwaagiza wananchi wa Itonjanda kuhakikisha kuwa Hosteli ililozinduliwa inapata wanafunzi wenye uhitaji wa kukaa shuleni, na wasipofanya hivyo atawaagiza wakuu wa shule wenye wasichana wanaohitaji Hosteli, kuhamia Itonjanda ili wafurahie fursa hiyo.

Kigoma Vijijini.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ester Mahawe alisema jitihada ambazo zimefanyika katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika Wilaya yake hazina lengo la kuwapendelea wasichana katika kupata elimu bali kuleta usawa kwa wote.

Mh. Mhawe amesema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla ya makabidhiano ya vyoo vya kisasa vya wasichana katika Shule za Msingi Ruhobe na Bitale ambayo vyote vina matundu 12, chumba maalumu Cha kujisitiri wasichana Pamoja na choo Cha wenye ulemavu.

Kila choo kimegharimu Tsh. Milioni 26 kila kimoja.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema “Kazi hii kubwa imefanywa na Serikali ikishirikiana na wadau wetu @HakiElimu kwa sababu msichana alikuwa ameachwa nyuma katika safari ya elimu, lengo ni kuleta usawa na sio kuwatenga watoto wa kiume. Tunawapenda sana watoto wa kiume” alisema DC Mahawe.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt.John Kalage alisema, Suala la kuwapa kipaumbele watoto wa kike halina maana ni kuwasahau watoto wa kiume bali fedha zilizopatikana zilikuwa na malengo kwa watoto wa kike, na ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali na Serikali ili kuhakikisha watoto wote wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kufundishiwa.

Korogwe.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basila Mwanukuzi aliahidi kuhakikisha maji yanafika kwenye shule ya Sekondari Mashewa ili kuwapunguzia kero ya maji wanafunzi wawapo masomoni.

Ahadi hiyo aliitoa alipozindua Bweni lenye uwezo wa kubeba wasichana 48 lililojengwa na Wananchi kwa msaada wa shirika la HakiElimu na limegharimu Tsh. Milioni 62 Kati ya Tsh. Milioni 70 zilizotengwa kwaajili ya mradi huo.

Mhe. Basila amesema jitihada wanazozifanya HakiElimu na wadau wengine zimechangia kuwapa fursa kubwa wasichana na Wilaya yake itaendela kushirikiana nao ili kuleta usawa katika safari ya Elimu kwa watoto wa Korogwe.

“Changamoto ni nyingi na mimi Kama mlivyosema kwenye risala nitaondoka na hii changamoto ya maji naichukua na nitaiwasilisha kwa injia wa maji ili shule pamoja na wananchi wawe wanufaika wa maji” alisema Basila Mwanukuzi.

Mkuu huyo wa Wilaya pia alisema imefika wakati sasa ambapo jitihada kubwa zilizofanywa kwa watoto wa kike pia zielekezwe kwa watoto wa kiume ambao nao wameanza kurudi nyuma kwa kile kinachoonekana upendeleo kwa wasichana.

“Sasa hivi wanawake tuna nguvu sana kiasi kwamba wanaume nao wanarudi nyuma, nafasi yenu wanaume ipo pale pale, nimeteta na Mkurugenzi wa HakiElimu hapa, nikamwambia kweli tunafanya mambo mengi kumwezesha msichana kwa sababu amepata changamoto kubwa, lakini tusisahau wavulana.

“Kwa upendo huo huo ambao wasichana tunajengewa, pia hatuachi kuwatahmini na kuwasaidia watoto wa kiume, hawa wanaenda kuwa Baba, na tunaambiwa baba ndiye kichwa cha familia, kwa hiyo katika elimu lazima tujenge misingi bora pia ya kuwawezesha watoto wa kiume, katika misingi ya kimaadili na kiungozi, waweze kujiamini, wakati mwanawake anahamasika sana basi na wao wakahamasika ili jamii iwe na wananchi bora wenye uwezo wa kiakili kimwili na kiroho na waweze kutenda mema” Alisema DC Basila.

Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt. John Kalage alisema ufanisi wa utekelezwaji wa mradi huo wa AGE ulikuwa mahsus kwa mtoto wa kike, ila umewapa changamoto ya namna ya kuhakikisha wanakuja na mikakati ambayo haitamwacha nyuma mtoto wa kiume kwenye safari ya Elimu.

Mbali na Bweni la wasichana Shule ya Sekondari Mashewa Wilayani Korogwe, HakiElimu pia ilishirikiana na Wananchi kujenga Choo Cha kisasa chenye matundu 12 chenye chumba maalumu Cha kujisitiri wasichana wakiwa Hedhi pamoja na chumba Cha wenye ulemavu na choo Hiki kimegharimu Takriban Tsh. Milioni 25.

Miradi yote ya AGE Kwenye Wilaya zote Tano za Mpwapwa, Iramba, Tabora Manispaa, Kigoma Vijinini na Korogwe Imegharimu Takribani Tsh Milioni 300.

Back To Top