skip to Main Content
+255754 354681 info@hakielimu.or.tz

GAWE 2021

Asasi za kiraia zaidi ya 15, ikiwemo HakiElimu, pamoja na Halmashauri 9 za Mkoa waMara zinashiriki kwenye maadhimisho ya Juma la Elimu yanafanyika katika mji wa Shirati, Wilaya ya Rorya mkoani Mara kuanzia Mei 31 hadi June 4. Madhimisho hayo yanayoongozwa na kauli mbiu ya Uwekezaji katika Mifumo ya Elimu kwa Maendeleo Endelevu, yanalengakuzitafakari kwa kina changamoto za elimu na kwa pamoja kupanga mikakati ya kuzitatua. kuhakikisha utolewaji wa elimu bora na utakao mjengea mtoto maarifa na ujuzi wa kupambana kimaisha na hasa mtoto wa kike ambaye jamii nyingi humsahau.

Maadhimisho ya Juma la Elimu hufanyika kila mwaka duniani kote tangu 2003 yakiwa na lengo la kutoa fursa kwa kampeni za kitaifa na kikanda kuhusu elimu kuangazia kwa kina eneo mojawapo la agenda ya Elimu kwa Wote. Mwaka 2016 makubaliano yalifanyika ya kuweka msisitizo kwenye eneo la uwekezaji katika elimu ili kuchagiza ufikiwaji wa lengo namba nne la Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Mtandao wa Elimu Tanzania TEN/MET umekuwa ukiratibu maadhimisho haya tangu mawaka 2007.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania @tenmet Ochola Wayoga malengo mahususi ya madhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa umma juu ya madai ya haki ya elimu iliyo bora; kuhamasisha serikali kuzingatia makundi yaliyokosa fursa kama watoto wenye ulemavu, watoto wa kike. Lengo linguine mahususi ni kuboresha miundombinu na kuhamasisha na kukumbusha jamii, serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali wa elimu kuhusu umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika masuala ya elimu kwa kuimarisha mifumo ya elimu na kuwekeza katika TEHAMA

Katika maadhimisho haya kutakuwa na Kongamano la Elimu siku ya Alhamis Juni 3 ambapo wadau wa elimu pamoja na viongozi mbalimbali watashiriki. Mkuu wa Mkoa wa Mara Eng. Robert Gabriel ndiye amezindua maadhimisho haya na kuahidi kuendelea kushirikiana na asasi za kiraia ili kuleta maendeleo ya Elimu.

Amesema licha Serikali Kuwa na jukumu la msingi la utoaji wa huduma za jamii, ikiwemo elimu bora, bado Serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu. Amesema waraka wa elimu Na.3 na Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 vinabainisha nafasi ya kila mdau katika utoaji wa elimu.

“Ni fursa ya kipekee Juma la Elimu mwaka huu kuwa na ujumbe wa kuhimizana katika uwekezaji kwenye mifumo ya elimu ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu. Niwahakikishie usalama wenu pamoja na mali zenu, fanyeni kazi zenu bila wasiwasi, Mkoa wetu wa Mara ni sehemu salama sana. Lakini pia niwakaribisheni katika Mkoa wetu ili muweze kuwekeza na msiache kuchukua tahadhari dhidi ya Korona” alimaliza Eng Gabriel.

 

Back To Top